Ezekiel 23

Dada Wawili Makahaba

1Neno la Bwana likanijia kusema: 2 a“Mwanadamu, walikuwepo wanawake wawili, binti wa mama mmoja. 3 bWakawa makahaba huko Misri, wakajitia kwenye ukahaba tangu ujana wao. Katika nchi ile vifua vyao vya ubikira vikakumbatiwa huko na wakapoteza ubikira wao. 4 cMkubwa aliitwa Ohola na mdogo wake Oholiba. Walikuwa wangu nao wakazaa wavulana na msichana. Ohola ni Samaria, Oholiba ni Yerusalemu.

5 d“Ohola akajitia kwenye ukahaba alipokuwa bado ni wangu, akatamani sana wapenzi wake, mashujaa Waashuru, 6waliovaa nguo za buluu, watawala na majemadari, wote walikuwa wanaume vijana wa kuvutia, wapandao farasi. 7 eAkafanya ukahaba na wasomi wote wa Ashuru, na kujinajisi kwa sanamu zote za kila mwanaume aliyemtamani. 8 fHakuacha ukahaba wake aliouanza huko Misri, wakati ambapo tangu ujana wake wanaume walilala naye, wakikumbatia kifua cha ubikira wake na kumwaga tamaa zao juu yake.

9 g“Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa wapenzi wake, Waashuru, kwa kuwa ndio aliowatamani. 10 hWakamvua nguo zake wakamwacha uchi, wakawachukua wanawe na binti zake, naye wakamuua kwa upanga. Akawa kitu cha kudharauliwa miongoni mwa wanawake na adhabu ikatolewa dhidi yake.

11 i“Oholiba dada yake aliliona jambo hili, lakini kwa tamaa zake na ukahaba wake, akaharibu tabia zake kuliko Ohola dada yake. 12 jYeye naye aliwatamani Waashuru, watawala na majemadari, mashujaa waliovalia sare, wapandao farasi, wanaume vijana wote waliovutia. 13 kNikaona kuwa yeye pia alijinajisi, wote wawili wakaelekea njia moja.

14 l“Lakini yeye akazidisha ukahaba wake. Akaona wanaume waliochorwa ukutani, picha za Wakaldayo
Wakaldayo yaani Wababeli .
waliovalia nguo nyekundu,
15 nwakiwa na mikanda viunoni mwao na vilemba vichwani mwao, wote walifanana na maafisa wa Babeli wapandao magari ya vita, wenyeji wa Ukaldayo.
Ukaldayo yaani Babeli .
16 pMara tu alipowaona, aliwatamani, akatuma wajumbe kwao huko Ukaldayo. 17 qNdipo hao Wababeli wakaja kwake kwenye kitanda cha mapenzi, nao katika tamaa zao wakamtia unajisi. Baada ya kutiwa unajisi, akawaacha kwa kuwachukia. 18 rAlipofanya ukahaba wake waziwazi na kuonyesha hadharani uchi wake, nilimwacha kwa kumchukia, kama vile nilivyokuwa nimemwacha dada yake. 19 sLakini akazidisha zaidi ukahaba wake alipozikumbuka siku zake za ujana, alipokuwa kahaba huko Misri. 20 tHuko aliwatamani wapenzi wake, ambao viungo vyao vya uzazi ni kama vya punda, na kile kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi. 21 uHivyo ulitamani uasherati wa ujana wako wakati ulipokuwa Misri, kifua chako kilipokumbatiwa, na walipokutomasa kwa sababu ya matiti yako machanga.

22 v“Kwa hiyo, Oholiba, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitawachochea wapenzi wako wawe kinyume na wewe, wale uliowaacha kwa kuchukia, nitawaleta dhidi yako kutoka kila upande: 23 wWababeli na Wakaldayo wote, watu kutoka Pekodi, na Shoa na Koa, wakiwa pamoja na Waashuru wote, vijana wazuri, wote wakiwa watawala na majemadari, maafisa wa magari ya vita na watu wa vyeo vya juu, wote wakiwa wamepanda farasi. 24 xWatakuja dhidi yako wakiwa na silaha, magari ya vita, magari ya kukokota, pamoja na umati mkubwa wa watu. Watakuzingira pande zote kwa ngao na vigao na kofia za chuma. Nitakutia mikononi mwao ili wakuadhibu, nao watakuadhibu sawasawa na sheria zao. 25 yNitaelekeza wivu wa hasira yangu dhidi yako, nao watakushughulikia kwa hasira kali. Watakatilia mbali pua yako na masikio yako, na wale watakaosalia miongoni mwako watauawa kwa upanga. Watachukua wana wako na binti zako, na wale watakaosalia miongoni mwenu watateketezwa kwa moto. 26 zWatakuvua pia nguo zako na kuchukua mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito na dhahabu. 27 aaHivyo ndivyo nitakavyokomesha uasherati wako na ukahaba wako uliouanza huko Misri. Hutatazama vitu hivi kwa kuvitamani tena, wala kukumbuka Misri tena.

28 ab“Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ninakaribia kukutia mikononi mwa wale unaowachukia, kwa wale uliojitenga nao kwa kuwachukia. 29 acWatakushughulikia kwa chuki na kukunyang’anya kila kitu ulichokifanyia kazi. Watakuacha uchi na mtupu na aibu ya ukahaba wako itafunuliwa. Uasherati wako na uzinzi wako 30 adumekuletea haya yote, kwa sababu ulitamani mataifa na kujinajisi kwa sanamu zao. 31 aeUmeiendea njia ya dada yako, hivyo nitakitia kikombe chake mkononi mwako.

32 af“Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: “Utakinywea kikombe cha dada yako,
kikombe kikubwa na chenye kina kirefu;
nitaletea juu yako dharau na dhihaka,
kwa kuwa kimejaa sana.

33 agUtalewa ulevi na kujawa huzuni,
kikombe cha maangamizo na ukiwa,
kikombe cha dada yako Samaria.

34 ahUtakinywa chote na kukimaliza;
utakivunja vipande vipande
na kuyararua matiti yako.

Nimenena haya, asema Bwana Mwenyezi.

35 ai“Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa tangu uliponisahau mimi na kunitupa nyuma yako, lazima ubebe matokeo ya uasherati wako na ukahaba wako.”

36 aj Bwana akaniambia, “Mwanadamu, Je, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi wakabili kwa ajili ya matendo yao ya machukizo, 37 akkwa kuwa wamefanya uzinzi na damu imo mikononi mwao. Wamefanya uzinzi na sanamu zao, hata wamewatoa watoto wao walionizalia kuwa kafara, kuwa chakula kwao. 38 alPia wamenifanyia hili: wakati huo huo wamenajisi patakatifu pangu na kuzitangua Sabato zangu. 39 amSiku ile ile walitoa watoto wao kuwa kafara kwa sanamu zao, waliingia patakatifu pangu na kupatia unajisi. Hilo ndilo walilolifanya katika nyumba yangu.

40 an“Walituma hata wajumbe kuwaita watu kutoka mbali, nao walipowasili ulioga kwa ajili yao, ukapaka macho yako rangi na ukavaa mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito vya dhahabu. 41 aoUkaketi kwenye kiti cha anasa, kukiwa na meza iliyoandaliwa mbele yake ambayo juu yake ulikuwa umeweka uvumba na mafuta ambayo yalikuwa yangu.

42 ap“Kelele za umati wa watu wasiojali zilikuwa zimemzunguka, wakaleta watu wengi waliokuwa wakifanya makelele na walevi kutoka nyikani, ambao walitia bangili kwenye mikono ya yule mwanamke na dada yake na pia taji nzuri za kupendeza kwenye vichwa vyao. 43 aqNdipo nikasema kuhusu yule aliyechakazwa na uzinzi, ‘Basi wamtumie kama kahaba, kwa kuwa ndivyo alivyo.’ 44Nao wakazini naye. Kama vile watu wazinivyo na kahaba, ndiyo hivyo walivyozini na hao wanawake waasherati, Ohola na Oholiba. 45 arLakini watu wenye haki, watawahukumia adhabu wanawake wafanyao uzinzi na kumwaga damu, kwa kuwa ni wazinzi na damu iko mikononi mwao.

46 as“Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo, Leteni watu wengi wenye makelele dhidi yao na uwaache wapate hofu na watekwe nyara. 47 atHao watu wengi watawapiga kwa mawe na kuwaua kwa panga zao, watawaua wana wao na binti zao na kuzichoma nyumba zao.

48 au“Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi, ili wanawake wote wapate onyo nao wasije wakafanya uasherati kama ninyi mlivyofanya. 49 avUtapata adhabu kwa ajili ya uasherati wako na kuchukua matokeo ya dhambi zako za uasherati. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.”
Copyright information for SwhKC